9 Aprili 2025 - 21:13
Source: IQNA
Wairani 192,000 wameshiriki ibada ya Umrah katika duru ya awali

Awamu ya kwanza ya safari ya Umrah kwa Mahujaji kutoka Iran kwa mwaka huu imehitimishwa rasmi, ambapo takriban Wairani 192,000 wametekeleza ibada hiyo tukufu ya Hijja Ndogo nchini Saudi Arabia.

Kwa mujibu wa maafisa wa Kiirani, awamu hii ya mwanzo ilianza tarehe 18 Septemba, 2024 na inatarajiwa kuwa Mahujaji wa Umrah wote watarejea nchini Iran kufikia tarehe 22 Aprili, 2025, InshaAllah.

Hivi sasa, Saudi Arabia iko katika maandalizi ya Ibada ya Hija ya kila mwaka – tukio la kiroho linalowakusanya Waislamu kutoka kila pembe ya dunia, wakielekea katika miji mitakatifu ya Makka na Madina kwa ajili ya kutekeleza nguzo ya tano ya Uislamu.

Baada ya mapumziko mafupi ya takriban wiki mbili kupisha Mahujaji wa Hija ya Faradhi awamu ya pili ya safari za Umrah kwa Wairani inatarajiwa kuanza tena katikati ya mwezi Julai 2025, mara tu baada ya kukamilika kwa ibada za Hajj.

Msimu huu wa Umrah umeashiria hatua muhimu katika mahusiano ya kidiplomasia kati ya Iran na Saudi Arabia, kwani huu ndiyo msimu wa kwanza mkubwa wa Umrah kwa Wairani tangu mwaka 2016.

Kusitishwa kwa safari hizo kulifuatia mvutano wa kidiplomasia na kukatika kwa uhusiano rasmi baina ya mataifa hayo mawili ya Kiislamu. Hata hivyo, mwezi Machi 2023, Iran na Saudi Arabia zilifikia makubaliano ya kurejesha uhusiano wao kupitia upatanishi wa Jamhuri ya Watu wa China – hatua ambayo ilifungua mlango wa ushirikiano mpya, ikiwemo katika sekta ya utalii wa kidini.

Mapema mwaka huu, Taasisi ya Hija na Umrah ya Iran ilitangaza kuwa zaidi ya Wairani 200,000 wanatarajiwa kushiriki katika Umrah kufikia mwisho wa msimu huu wa safari za kidini.

Umrah, tofauti na Hija ya Faradhi, ni ibada inayoweza kutekelezwa wakati wowote wa mwaka, na si ya lazima, lakini inapendekezwa sana katika mafundisho ya Kiislamu. Ni fursa ya kumkaribia Mwenyezi Mungu, kujitakasa kiroho, na kuimarisha uhusiano wa muumini na nyumba yake.

342/

Your Comment

You are replying to: .
captcha